Emmanuel Khaingah: Sammy Ondimu Akutana na Jamaa Aliyemwokoa Polisi, Amzawadia KSh 5,000

Emmanuel Khaingah: Sammy Ondimu Akutana na Jamaa Aliyemwokoa Polisi, Amzawadia KSh 5,000

  • Afisa wa polisi alikuwa miongoni mwa waathiriwa wa maandamano ya fujo yaliyofanyika tarehe 25 Juni katika jiji la Nairobi
  • Konstebo wa Polisi Emily Kinya alishambuliwa na waandamanaji waliompiga kabla ya kijana mmoja kujitokeza na kumwokoa
  • Emmanuel Khainga ndiye aliyemwokoa, akijitosa katika hasira ya waandamanaji ili kuokoa maisha ya afisa huyo; Wakenya walithamini kitendo chake kwa zawadi za pesa

Afisa wa polisi Sammy Ondimu ametimiza ahadi yake kwa kijana aliyemwokoa askari mwanamke kutoka kwa umati wenye hasira.

Emmanuel Khaingah: Sammy Ondimu Akutana na Jamaa Aliyemwokoa Polisi, Amzawadia KSh 5,000
Afisa wa polisi Sammy Ondimu akiwa na Emmanuel Khainga jijini Nairobi.
Chanzo: UGC

Emmanuel Khaingah alivutia nyoyo za Wakenya baada ya kujitolea kumlinda askari wa kike aliyekuwa amezingirwa wakati wa maandamano ya Juni 25.

Kijana huyo jasiri alikabiliana na hasira ya umati na kusimama kati ya Police Konstebo Emily Kinya na watu waliokuwa wakimdhulumu, hali iliyosababisha majeraha yaliyompelekea kulazwa hospitalini mara moja.

Kitendo hicho cha ushujaa kilimvutia afisa mashuhuri Ondimu, ambaye aliahidi kumshukuru.

Afisa huyo anayehudumu Nakuru alipanga mkutano wa chakula cha mchana na Khaingah jijini Nairobi siku ya Alhamisi, Julai 3.

"Ninapatana na Emmanuel katika Expressway. Yuko nami na tuko live kwenye Facebook ili msikie kutoka kwake na kuelewa kilichomsukuma kufanya alichofanya," alisema Ondimu kupitia TUKO.co.ke.

Baadaye Wakenya walimzawadia Khaingah pesa taslimu video ya tukio hilo ilipoanz kusambaa mitandaoni kupitia ukurasa wa Facebook wa Ondimu.

Afisa huyo alitimiza ahadi yake ya kumpa KSh 5,000 kama shukrani, na hadhira ikaongeza zawadi hiyo wakisherehekea hatua ya haraka ya Khaingah kuokoa maisha ya askari huyo.

Akizungumza na TUKO.co.ke, askari wa kike Emily Kinya alithamini sana hatua ya haraka aliyochukua kijana huyo.

Alisema kama si yeye, maisha yake yangekuwa hatarini.

"Ninamshukuru sana. Kama si yeye, leo tungekuwa tunazungumza habari tofauti kabisa. Wakati mwingine maneno hayawezi kutosha, lakini ninamshukuru sana... Yeye ni shujaa," alisema Kinya, akiahidi kukutana na Khaingah pindi atakapopona.

Kwa upande wake, Khaingah alisema aliongozwa na utu kumsaidia Kinya wakati wa dharura.

Kwa mtazamo wake, si polisi wote ni wakatili, kwani anawajua wengi ambao ni wakarimu na wapo tayari kusaidia wakati wowote.

Emmanuel Khaingah: Sammy Ondimu Akutana na Jamaa Aliyemwokoa Polisi, Amzawadia KSh 5,000
Emmanuel Khainga alisifiwa kwa ushujaa wake alipoingia kuokoa polisi mwanamke aliyekuwa akishambuliwa na waandamanaji. Picha: Sammy Ondimu.
Chanzo: Facebook

Ondimu alitumia nafasi hiyo kuendeleza kampeni yake ya kuimarisha uhusiano mzuri kati ya wananchi na polisi.

Alikiri kwamba ndani ya idara ya polisi, wapo wachache wanaokiuka maadili na kuharibu sura ya maafisa wengine wanaotekeleza majukumu yao kwa heshima na upole.

Kwa nini Wakenya huwaona polisi kama maadui

Kwa muda mrefu, sehemu kubwa ya Wakenya wamekuwa na chuki dhidi maafisa wa polisi kutokana na mienendo yao kazini.

Polisi wamewahi kunaswa katika matukio kadhaa ya ukatili dhidi ya raia, hali inayozorotesha matumaini ya upatanisho.

Kisa cha hivi karibuni kilichoibua hasira ni mauaji ya Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi.

Ojwang alikamatwa Juni 7 huko Homa Bay County na kusafirishwa hadi Nairobi County, ambako alizuiliwa kwa muda katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi alipouwawa.

Tukio hilo liliibua hasira miongoni mwa Wakenya waliomiminika mitaani kuonyesha kutoridhishwa kwao na utendakazi wa polisi.

Na wakati umma ulikuwa mitaani mnamo Juni 18, Mkenya mwingine aliyekuwa akiuza barakoa alishambuliwa kwa ukatili na kupigwa risasi hadi kufa na polisi aliyekuwa akidhibiti maandamano.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »