Mtandao wa X Wazimwa Tanzania Baada ya Rais Kuzushiwa Kifo, NetBlocks Wanaripoti

Mtandao wa X Wazimwa Tanzania Baada ya Rais Kuzushiwa Kifo, NetBlocks Wanaripoti

  • Tanzania kwa mara nyingine tena imezima mtandao wa kijamii wa X, kufuatia kudukuliwa kwa akaunti muhimu ya serikali ambayo imetumiwa kueneza uvumi kuhusu kifo cha Rais Samia Suluhu Hassan
  • Kikundi cha ufuatiliaji wa masuala ya mtandaoni cha NetBlocks kilithibitisha hatua hiyo, wakisema kuwa watoa huduma wote wakuu wa intaneti nchini wameathirika
  • Kuzimwa huko kwa huduma kumewasha wasiwasi kuhusu mwenendo unaoendelea wa kuongezeka kwa udhibiti wa serikali na ukandamizaji mkali wa uhuru wa kujieleza mtandaoni nchini Tanzania

Tanzania imekata tena huduma ya mtandao wa kijamii wa X (uliokuwa ukiitwa Twitter), miezi michache tu baada ya tukio sawa na hilo.

Mtandao wa X Wazimwa Tanzania Baada ya Rais Kuzushiwa Kifo, NetBlocks Wanaripoti
Ufikiaji wa jukwaa la X nchini Tanzania umezuiwa kufuatia madai ghushi kuhusu kifo cha Rais Samia Suluhu. Picha: Nicolas Guyonnet/Getty Images, Samia Suluhu.
Chanzo: UGC

Hatua hiyo ya hivi punde ilikuja baada ya shambulio la mtandaoni, ambalo lilishuhudia akaunti rasmi ya Jeshi la Polisi Tanzania ikidukuliwa na kutumiwa kusambaza taarifa za uongo zinazodai kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefariki dunia.

Kikundi cha ufuatiliaji wa masuala ya mtandao cha NetBlocks kilithibitisha kuwa mfumo huo umezimwa kwa watoa huduma wote wakuu wa intaneti kote Tanzania.

Katika taarifa kwenye X, NetBlocks ilieleza kuwa data ya moja kwa moja ilionyesha mtandao uliokuwa umezimwa nchini Tanzania.

"Vipimo vya moja kwa moja vinaonyesha X (zamani Twitter) imekuwa haipatikani kwa watoa huduma wakuu wa mtandao nchini #Tanzania; tukio hilo linakuja wakati akaunti ya polisi iliyoathiriwa ikidai kuwa Rais amefariki, jambo linaloukasirisha uongozi wa nchi."

Kwa nini mtandao wa X amezimwa Tanzania?

Kisa hicho kilitokea siku chache baada ya rais kuagiza polisi kuimarisha ulinzi kwenye mitandao ya kijamii, na kuangazia umuhimu wa kulinda maslahi ya taifa katika nyanja ya kidijitali.

Mapema mwezi wa Mei, Tanzania iliondoa zaidi ya tovuti 80,000, akaunti za mitandao ya kijamii, blogu na majukwaa mengine ya mtandaoni katika kile kilichochukuliwa kuwa ukandamizaji mkubwa zaidi wa maudhui ya kidijitali katika historia ya nchi.

Ingawa serikali ilisisitiza hatua inayolenga kulinda ustawi wa kiakili wa watoto, pia iliangazia mwelekeo unaoongezeka wa udhibiti mkali wa mtandaoni.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwijuma, aliliambia Bunge kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza majukwaa 80,171 kwa kusambaza maudhui yasiyo ya kimaadili yanayotishia afya ya akili ya watoto.

Mwijuma aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum Ng’wasi Kamani kuhusu mkakati wa serikali wa kudhibiti maudhui ya mitandao ya kijamii.

Utekelezaji huu mkubwa ulikuwa sehemu ya juhudi pana za serikali ambazo zimekuwa zikiendelezwa katika muongo mmoja uliopita.

Mwaka 2017, Tanzania ilitunga kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta (yaliyomo mtandaoni), ambazo zilifanyiwa marekebisho zaidi mwaka 2020.

Sheria hizi zinaharamisha maudhui yanayoonekana kuwa yasiyofaa, machafu, chuki, au yanayoweza kuvuruga amani ya umma.

Wakiukaji wanaweza kufungwa jela hadi miezi 12, kutozwa faini ya TSH 5 milioni (takriban KSh 238,860), au zote mbili. Kanuni hizo ziliipa TCRA mamlaka makubwa ya kufuatilia na kudhibiti mitandao ya kijamii, zikiwemo blogu na akaunti za mtumiaji binafsi.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Francis Silva avatar

Francis Silva (Swahili translator) Francis M Silva ni Mkuu wa Kitengo cha Kiswahili. Ana tajriba ya miaka mingi katika taaluma ya uwanahabari hasa tafsiri, uhariri - Radio, TV na Dijitali. Yeye ni zao la Taasisi ya Mawasiliano-Umma ya Kenya (KIMC). Wasiliana naye kupitia: [email protected]

OSZAR »