Zimbabwe Yaonya Raia Kuhusu Ukurasa wa Facebook wa Kenya Unaoahidi Kazi Feki

Zimbabwe Yaonya Raia Kuhusu Ukurasa wa Facebook wa Kenya Unaoahidi Kazi Feki

  • Raia wa Zimbabwe wameonywa baada ya ukurasa wa Facebook kujitangaza kama ubalozi wa Kenya ukitoa ofa feki za kazi
  • Waathiriwa walitakiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya cheti ghushi cha kazi kama sehemu ya kashfa hiyo
  • Tahadhari hiyo ilikuja huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ulaghai wa kazi mtandaoni unaolenga watu wanaotafuta kazi waliokata tamaa

Ukurasa wa Facebook uliojitambulisha kama ya ubalozi uligeuka kuwa mtego wa kidijitali kwa wanaotafuta kazi waliokata tamaa.

zimbabwe
Wizara ya mambo ya nje ya Zimbabwe ilionya kuhusu ukurasa ghushi wa Facebook. Picha ya kwanza kwa kielelezo. Picha: South Agency/Getty Images, @MOFA_ZW.
Chanzo: UGC

Hivi majuzi serikali ya Zimbabwe ilitoa tahadhari ya dharura ikiwaonya raia wake kuhusu kashfa ghushi ya kuajiri watu wanaotafuta kazi mtandaoni.

Ulaghai huo, ambao ulifanyika hasa kupitia Facebook, ulidai kwa uwongo kutoa nafasi za ajira nchini Kenya na tayari ulikuwa umewavutia waathiriwa ambao hawakuwa na wasiwasi kabla ya mamlaka kuingilia kati.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa, mpango huo wa ulaghai ulikuwa ukiendeshwa kupitia ukurasa wa Facebook unaoitwa Ubalozi wa Zimbabwe Kenya.

Je, kashfa ya kazi ya Zimbabwe ilifanyaje kazi?

Ukurasa huo, ulioundwa Juni 14 na watu wasiojulikana, ulijifanya kama jukwaa rasmi la ubalozi na ulidai kwa uongo kuwa unashughulikia uajiri wa Wazimbabwe nchini Kenya.

Kama sehemu ya ulaghai huo, waombaji kazi walitakiwa kulipa $375 (takriban KSh 48,000), kwa kile kilichoelezwa kama "Cheti cha Ithibati ya Kazi ya Kanda ya Afrika" - sharti ambalo serikali ilithibitisha halipo.

Wizara hiyo ilifafanua kuwa hakuna mchakato halali wa kazi wa serikali unaohusisha aina yoyote ya malipo.

Uajiri rasmi unashughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Umma ya Zimbabwe na daima ni bure.

Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na msemaji wa wizara hiyo, ilisisitiza zaidi kwamba ukurasa huo wa ulaghai hauna uhusiano wowote na Ubalozi wa Zimbabwe nchini Kenya, Wizara yenyewe, au taasisi yoyote ya serikali inayotambuliwa.

Zimbabwe ilisema nini kuhusu ukurasa ghushi wa Kenya wa Facebook?

Wananchi walihimizwa kupuuza ofa hizo na kuepuka kushiriki habari za kibinafsi au za kifedha mtandaoni.

Wizara ilionya kuwa zaidi ya hasara ya kifedha, waathiriwa wa ulaghai kama huo wanaweza pia kukabiliwa na wizi wa utambulisho na hatari zingine.

Ilitoa wito kwa Wazimbabwe kuwa waangalifu wanapotafuta kazi mtandaoni na kuwashauri kuthibitisha fursa moja kwa moja kupitia tovuti rasmi za serikali au mawasiliano ya ubalozi.

Onyo hili linakujia huku kukiwa na ongezeko la wasiwasi katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kuhusu ulaghai wa kazi mtandaoni kuwa wa hali ya juu na vigumu kutambulika.

Walaghai wengi sasa wanaiga chapa, lugha na taratibu za taasisi halisi ili zionekane kuwa halali, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa mtu wa kawaida kutofautisha.

zimbabwe
Ofisi ya wizara ya mambo ya nje na biashara ya kimataifa ya Zimbabwe. Picha: MOFAIT.
Chanzo: Facebook

Kwa nini mashirika ya uajiri ya Eldoret yalikabiliwa na mtikisiko mkubwa?

Katika tukio linalohusiana na hilo lililoripotiwa awali na TUKO.co.ke, mamlaka ya Kenya ilianzisha msako dhidi ya mashirika ya kuajiri watu katika kaunti ya Uasin Gishu.

Mashirika hayo yote yaliamuriwa kusitisha shughuli na kutuma maombi ya leseni mpya kufuatia malalamishi kutoka kwa wenyeji waliosema walidanganywa na ofa za kazi ghushi nje ya nchi.

Kamishna wa Kaunti hiyo, Eddyson Nyale, alisema uamuzi huo ulifuatia mashauriano na Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri na unalenga kusafisha sekta hiyo.

Mashirika ya usafiri yanayojifanya kuajiri kwa kazi za ng'ambo pia yalikumbwa na msukosuko huo, huku serikali ikizidisha juhudi za kulinda umma dhidi ya udanganyifu na unyonyaji.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »