Musalia Mudavadi Athibitisha Boniface Mwangi Anazuiliwa Tanzania Kufuatia Ripoti Ametoweka

Musalia Mudavadi Athibitisha Boniface Mwangi Anazuiliwa Tanzania Kufuatia Ripoti Ametoweka

  • Waziri Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, amethibitisha kuwa mwanaharakati Boniface Mwangi anazuiliwa na mamlaka za Tanzania
  • Mudavadi alisema kuwa ubalozi wa Kenya uko katika mawasiliano na Mwangi kuhusiana na hali yake
  • Mwangi alisafiri hadi Tanzania kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, na alikamatwa Jumatatu, Mei 19
  • Mwanaharakati wa haki za binadamu, Hussein Khalid, alipiga kams akisema kuwa Mwangi pamoja na mwandishi wa habari kutoka Uganda, Agatha Atuhaire, hawajulikani waliko licha ya madai kuwa walifukuzwa nchini

Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Musalia Mudavadi amethibitisha kuwa mwanaharakati Boniface Mwangi yuko chini ya ulinzi wa mamlaka ya Tanzania.

Musalia Mudavadi Athibitisha Boniface Mwangi Anazuiliwa Tanzania Kufuatia Ripoti Ametoweka
Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi na mwanaharakati Boniface Mwangi katika matukio ya awali. Picha: Musalia Mudavadi/Boniface Mwangi.
Chanzo: Twitter

Mudavadi alisema kuwa ubalozi wa Kenya jijini Dar es Salaam umekuwa katika mawasiliano na Boniface Mwangi na unafanya juhudi za dhati kubaini jinsi atakavyosaidiwa kuachiliwa na kurejeshwa Nairobi.

Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV siku ya Jumanne, Mei 20, alikiri kuwa serikali ya Tanzania haijatoa maelezo ya wazi kuhusu sababu za kukamatwa kwa Mwangi au kuhusu uhamisho wa hivi majuzi wa raia kadhaa wa Kenya.

“Boniface Mwangi yuko Tanzania na anazuiliwa na mamlaka. Tunatumaini ataachiliwa na kusaidiwa kurudi nyumbani,” alisema Mudavadi.

“Nadhani watu waliotembelea Tanzania waliitikisa serikali ya huko hasa katika kipindi hiki kigumu na chenye hisia kali za uchaguzi,” aliongeza Waziri wa Mambo ya Nje.

Mwangi alikuwa amesafiri hadi Dar es Salaam kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani wa Tanzania, Tundu Lissu.

Kabla ya kukamatwa kwake siku ya Jumatatu, Mei 19, mwanaharakati huyo aliripoti kuwa maisha yake yalikuwa hatarini baada ya wanaume wenye silaha kuizingira chumba chake katika Hoteli ya Serena.

Mapema siku ya Jumanne, Mei 20, rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alithibitisha kuwa Mwangi na mwandishi wa habari na wakili kutoka Uganda, Agatha Atuhaire, walikuwa tayari wamefukuzwa nchini humo.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, kufukuzwa kwao kulisimamiwa na Idara ya Uhamiaji ya Tanzania.

Mwangi na Atuhaire waliripotiwa kuzuiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam tangu kukamatwa kwao siku ya Jumatatu, Mei 19.

Ilidaiwa kuwa Mwangi alikamatwa kwa madai ya kutoa taarifa za uongo ili kuingia nchini Tanzania.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kujitokeza na kuthibitisha usalama wao, mwanaharakati wa haki za binadamu Hussein Khalid alipiga kamsa, akisema kuwa juhudi za kuwatafuta Mwangi na Atuhaire kupitia njia za kisheria na kidiplomasia ziligonga mwamba, jambo lililozua wasiwasi kuhusu usalama na mahali walipo.

Musalia Mudavadi Athibitisha Boniface Mwangi Anazuiliwa Tanzania Kufuatia Ripoti Ametoweka
Boniface Mwangi alizuiliwa nchini Tanzania kufuatia kukamatwa kwake Jumatatu, Mei 19. Picha: Hussein Khalid.
Chanzo: Twitter

Kisa hiki kinatokea wakati ambapo kuna msisimko wa kidiplomasia katika eneo hili kufuatia kuzuiliwa na kufukuzwa kwa Wakenya wengine mashuhuri, akiwemo mwanasiasa Martha Karua na aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, waliokuwa wameenda Tanzania kuonyesha mshikamano wao na Tundu Lissu.

Serikali ya Kenya bado haijatoa tamko rasmi la kidiplomasia, huku Mudavadi akisema kuwa uchunguzi kuhusu suala hilo bado unaendelea.

Mengi kufuata...

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »