Allois Cheruiyot Bett: Kasisi Apigwa Risasi Siku chache baada ya Mwingine Kupatikana Ameuawa
- Padre Allois Cheruiyot Bett wa Parokia ya St. Matthias Mulumba Tot aliuwawa siku ya Alhamisi, Mei 22
- Katika taarifa iliyotolewa na Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Padre Allois alivamiwa na watu waliokuwa wamejihami katika eneo la Mokoro, kata ndogo ya Kakiptul
- Wakenya wamemtaja Padre Allois, ambaye alikuwa akihudumu chini ya Jimbo Katoliki la Eldoret, kama mtumishi mwaminifu wa Mungu, mtu mwenye huruma, na nguzo ya tumaini kwa watu wengi
PAY ATTENTION: Flexible Payment Plans Available! Invest in Yourself & See the Return with Our Affordable Copywriting Course!
Elgeyo Marakwet – Jumuiya ya Wakatoliki imeingia katika maombolezo kufuatia kifo cha kusikitisha cha Padre Allois Cheruiyot Bett.

Chanzo: Facebook
TV 47 iliripoti kuwa Padre Allois wa Jimbo Katoliki la Eldoret alivamiwa na kuuawa na watu wasiojulikana siku ya Alhamisi, Mei 22, akiwa katika shughuli zake za kichungaji katika eneo la Tot.
Akithibitisha taarifa hiyo ya kusikitisha, Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ilisema kuwa Padre Allois alivamiwa na watu waliokuwa na silaha katika eneo la Mokoro, kata ndogo ya Kakiptul.
“Tungependa kuthibitisha kwa masikitiko tukio la kusikitisha la kupigwa risasi kwa Padre Allois Cheruiyot Bett wa Parokia ya St. Matthias Mulumba Tot. Tukio hilo lilitokea katika Eneo la Mokoro, Kata Ndogo ya Kakiptul, Kijiji cha Kabartile. Maafisa wa Kikosi Maalum cha GSU walijibu haraka na kubaini kuwa Padre Bett alivamiwa na kupigwa risasi na watu waliokuwa wamejihami. Msako ulianzishwa mara moja, na washukiwa sita tayari wamekamatwa na wanazuiliwa," ilisema NPS.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Eldoret, John Kiplimo Arap Lelei, alisema kifo cha Padre Allois kimeacha pengo kubwa katika Jimbo Katoliki la Eldoret, kwani alikuwa mtumishi mwaminifu wa Mungu, mtu mwenye huruma, na nguzo ya tumaini kwa watu wengi.
Padre Allois alijulikana sana kwa uaminifu wake kwa imani ya Kikristo, huduma yake isiyochoka kwa jamii, na unyenyekevu wake.

Chanzo: Twitter
Wakenya walivyomuomboleza Padre Allois Cheruiyot Bett
Seneta wa Nandi, Kiprotich Arap Cherargei, ni miongoni mwa Wakenya waliomlilia Padre huyo. Katika ujumbe wake wa rambirambi, Cherargei alitoa wito kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuchukua hatua kali kumaliza uhalifu wa wavamizi wa silaha katika Bonde la Kerio.
"Rambirambi zangu za dhati kwa mauaji yasiyo na maana ya Rev. Fr. Alois Cheruiyot Bett na wavamizi wanaodaiwa katika Bonde la Kerio, Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Alikuwa akihudumu katika Jimbo Katoliki la Eldoret na anatoka Lessos katika eneobunge la Nandi Hills, Kaunti ya Nandi. Uhalifu huu unaendelea kugharimu maisha na amani, hali inayopaswa kushughulikiwa vikali na vyombo vya usalama tunapoendelea kuomba amani na utulivu katika eneo la Bonde la Kerio."
Maoni ya Wakenya mitandaoni:
Cheruto Cheruto: “Inasikitisha sana 💔. Tunalifunga pepo la mauti kwa jina la Yesu! Tunaombea kanisa la Kristo.”
Lindsey Ruth: “Haiaminiki… pumzika kwa amani Fr. Alois 😭.”
Laurrets Mitchelle: “Murkomen hafanyi kazi tena… ina maana kuwa wavamizi wana nguvu kuliko vikosi vya usalama? Au anaangazia Trans Nzoia tu?”
Je, Padre John Maina aliuawa?
Kifo cha Padre Allois kimetokea muda mfupi tu baada ya mauaji ya Padre John Maina kutoka Jimbo Katoliki la Nyahururu.
Kuuawa kwa Padre Maina kuliwashtua jamii za kidini na umma kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa kulitokea wiki tatu tu baada ya yeye kuwa mwenyeji wa naibu rais wa zamani Rigathi Gachagua pamoja na viongozi wengine mashuhuri katika harambee ya hadhi ya juu.
Mwili wake usio na uhai ulipatikana siku ya Alhamisi, tarehe 15 Mei, takribani kilomita 50 kutoka parokia yake ya Kanisa Katoliki la Igwamiti.
Wapelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wanashuku kuwa mauaji yalitokea eneo tofauti, kisha mwili wake kutupwa baadaye eneo la Kikopey, kandokando ya barabara kuu ya Nakuru-Nairobi karibu na Gilgil.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke