Magazeti ya Kenya, Mei 24: Serikali Yapanga Kuregesha Ada ya Mitihani Iliyofutwa Enzi ya Uhuru
Mnamo Jumamosi, Mei 24, magazeti ya humu nchini yalijadili masuala mbalimbali, yakisisitiza mabadiliko ya kisiasa nchini na maamuzi ya serikali yanayoathiri raia.

Chanzo: UGC
1. Saturday Nation
Gazeti hili liliripoti kuwa serikali inapanga kuondoa msamaha wa ada ya mitihani ya kitaifa ambao umekuwepo kwa miaka kumi, kuanzia mwaka ujao. Hii itawalazimu wazazi kulipia mitihani ya kitaifa ya watoto wao isipokuwa kwa wale watakaothibitishwa kuwa wahitaji kupitia mfumo maalum wa tathmini ya hali ya kiuchumi.
Waziri wa Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi, John Mbadi, alisema serikali itatumia mfumo wa ruzuku ya walengwa ili kuwasaidia tu wale wasioweza kumudu ada hizo. Hata hivyo, hakufafanua ni vigezo gani vitatumika kubaini uhitaji.
Mbadi alisema kuwa wazazi wanaolipia karo ya juu katika shule za binafsi wana uwezo wa kulipa ada ya mitihani, na akauliza kwa nini walipa kodi wachukue mzigo wa kugharamia mitihani ya kila mwanafunzi.
Msamaha huu ulianzishwa mwaka 2015 na Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta kwa shule za umma, na kupanuliwa hadi shule binafsi mwaka 2017, na umesaidia wanafunzi kufanya mitihani ya kitaifa kama KCSE, KPSEA na KJSEA bila malipo.
Serikali imeongeza ufadhili wa mitihani kutoka KSh4 bilioni hadi KSh5 bilioni kwa mwaka katika kipindi cha hivi karibuni.
Mbadi alitetea mabadiliko haya kama hatua ya kuwajibika kifedha na kuhakikisha haki, huku akikanusha uvumi kuwa hakuna fedha za kugharamia mitihani ya mwaka huu, na kuwahakikishia wazazi wasipanic.
Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, David Njeng’ere, aliunga mkono mfumo wa ufadhili wa mtu binafsi (per capita funding) badala ya ruzuku ya jumla, akisema ongezeko la idadi ya watahiniwa limekuwa changamoto kwa ufadhili.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi Kitaifa, Silas Obuhatsa, alieleza wasiwasi wake kuhusu hatua hiyo, akataka mashauriano ya umma yafanyike na akaonya kuwa baadhi ya watoto wanaweza kulazimika kuacha shule kwa sababu ya kushindwa kulipia ada ya mitihani.
Alifananishi mpango huo na ule tata wa ufadhili wa vyuo vikuu ulioanzishwa mwaka 2023, ambao umekuwa na changamoto za utekelezaji na kesi za kisheria.
2. The Saturday Standard
Kwa mujibu wa chapisho hili, wakati Kenya ilikuwa bado inakabiliana na athari za maandamano ya Gen Z ya mwaka uliopita, Rais William Ruto anadaiwa kuchukua hatua kimyakimya kuimarisha mamlaka ya Ofisi ya Mkuu wa Wafanyakazi na Mkuu wa Utumishi wa Umma (HOPS), nafasi ambayo wataalamu wa sheria wanasema haijatajwa katika Katiba.
Gazeti hili linaripoti, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali na nyaraka, kuwa mojawapo ya matukio tata zaidi ni uhamisho wa kimya wa Muhuri wa Umma kutoka kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu hadi kwa HOPS, Felix Koskei, huku kukiwa na madai ya utekaji na watu kupotea kwa nguvu.
Muhuri wa Umma, uliobainishwa katika Katiba ya Kenya kama ishara ya kitaifa, hutumika kuthibitisha nyaraka rasmi za serikali.
Wakosoaji wanasema kuwa kuondolewa kwa muhuri kutoka kwa mamlaka ya Mwanasheria Mkuu kunaweza kudhoofisha usimamizi wa kisheria na kufungua mlango kwa shughuli za serikali zisizo na uwazi na uwajibikaji.
Mwanasheria Mkuu wa zamani, Justin Muturi, anadaiwa alipinga hatua hiyo, na baadhi ya watu wa ndani wanadai kuwa hilo lilisababisha kuondolewa kwake.
Mrithi wake, Dorcas Oduor, alitoa majibu ya kutoeleweka alipohojiwa kuhusu mahali ulipo muhuri huo kwa sasa.
Amri ya Rais iliyotolewa mwezi Novemba 2023 ilitangaza kuwa HOPS ndiye sasa atakuwa mlinzi wa muhuri huo.
Wataalamu wa sheria kama Gitobu Imanyara na Willis Otieno walionya kuwa hatua hiyo huenda inakiuka vipengele vya Katiba na kuhatarisha mfumo wa kuangalia na kusawazisha madaraka.
Wakati huo huo, msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, alitetea uhamisho huo kuwa wa kisheria, ingawa taarifa zinazopingana baadaye ziliibua mashaka kuhusu msingi wake wa kisheria.
Wachambuzi wa kisiasa na wa sheria wanasisitiza kuwa kuweka ishara yenye nguvu mikononi mwa mteule wa rais ambaye hakupitishwa na Bunge wala hana msingi wa kikatiba kunaweza kudhoofisha imani ya umma na kusababisha changamoto kubwa za kisheria.
3. Taifa Leo
Gazeti hili la Kiswahili liliripoti kuwa maafisa wa upelelezi mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado, walimkamata afisa wa polisi aliyedaiwa kuwashambulia na kuwajeruhi wenzake wawili wakiwa kazini kituoni.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi iliyosajiliwa chini ya nambari ya kitabu cha matukio 27/22/05/2025, afisa huyo kutoka Kituo cha Polisi cha Athi River, Kaunti ya Machakos, alikamatwa awali na maafisa wa trafiki barabarani katika barabara ya Nairobi–Namanga kwa makosa mbalimbali ya trafiki lakini akawa mkaidi.
Afisa huyo anadaiwa alikuwa amelewa wakati wa tukio hilo na anakabiliwa na mashtaka ikiwa ni pamoja na kuendesha gari lisilo na bima, kuendesha akiwa amelewa, kukaidi maagizo ya afisa wa trafiki, na kupinga kukamatwa.
Baada ya kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kitengela kwa ajili ya taratibu za kawaida, inadaiwa alishambulia maafisa wawili waliokuwa kazini—mlezi wa seli na mlinzi wa kituo—na kuwasababishia majeraha.
Afisa mmoja alipata majeraha kichwani na mguuni (kushoto), huku mwingine akivunjika kidole kidogo mkononi (kulia). Wote walipelekwa hospitalini na kupewa fomu za P3 kusaidia katika kesi ya mashitaka.
Mtuhumiwa bado anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kitengela huku uchunguzi ukiendelea, na gari alilokuwa akiendesha limekamatwa.
4. Weekend Star
Kulingana na gazeti hili, mwanamume mmoja alikamatwa kwa madai ya kuvamia Kanisa Katoliki la Suneka, Kaunti ya Kisii, na kusababisha uharibifu wa mali yenye thamani ya zaidi ya KSh200,000, kwa mujibu wa ripoti za polisi.
Mamlaka zilisema mtuhumiwa aliingia katika eneo la kanisa hilo kwa kuruka uzio wa nje na kisha kuvunja milango kuingia ndani.
Akiwa ndani, anaripotiwa kuvunja viti vya plastiki 27, spika mbili za muziki, milango kadhaa na dirisha moja.
Polisi walieleza kuwa walinzi watatu waliokuwa kazini walijaribu kumzuia lakini wakakumbana na vurugu.
Mlinzi mmoja alipoteza meno matatu, huku mwingine akipata majeraha makubwa baada ya kupigwa kwa chuma. Mlinzi aliyejeruhiwa alipelekwa hospitalini na hali yake iliripotiwa kuwa imetulia.
Maafisa wa usalama waliitika wito wa msaada, walimdhibiti mtuhumiwa na kumpeleka mahabusu.
Mtuhumiwa pia alipata majeraha wakati wa purukushani hiyo na alipelekwa hospitalini.
Wachunguzi walisema wanapanga kufanya tathmini ya kiakili ili kubaini hali ya akili ya mtuhumiwa. Sababu ya shambulio hilo bado haijafahamika.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke