Mwanasiasa wa Tanzania Azuiliwa Mpakani, Anyimwa Kibali Kusafiri Kwenda Kenya: "Tutashinda"

Mwanasiasa wa Tanzania Azuiliwa Mpakani, Anyimwa Kibali Kusafiri Kwenda Kenya: "Tutashinda"

  • Kiongozi wa upinzani Tanzania Godbless Lema alisema maafisa wa uhamiaji katika kituo cha mpaka cha Namanga walimzuia kusafiri kwenda Kenya kwa ziara ya kimatibabu
  • Mbunge huyo wa zamani wa Arusha alisema alisubiri kwa zaidi ya saa nne kabla ya kuambiwa arudi nyumbani na kuripoti makao makuu ya uhamiaji Dodoma kwa maelekezo zaidi
  • Idara ya Uhamiaji Tanzania baadaye ilithibitisha kukamatwa kwa hati ya kusafiria ya Lema, lakini ilikanusha madai kuwa viongozi wa CHADEMA walikuwa chini ya marufuku ya kusafiri
  • Lema alikosoa kile alichokieleza kuwa ni hali mbaya ya ukandamizaji chini ya serikali ya Rais Samia Suluhu

Namanga: Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Godbless Jonathan Lema amezuiwa kuondoka nchini humo katika mzozo wa mpaka huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa ukandamizaji wa kisiasa.

Mwanasiasa wa Tanzania Azuiliwa Mpakani, Anyimwa Kiali Kuingia Kenya: "Tutashinda"
Godbless Jonathan Lema akihutubia katika mkutano wa kisiasa uliopita. Picha: Global P.
Chanzo: Facebook

Godbless Lema ni nani?

Lema ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alizuiwa na maofisa wa uhamiaji katika Kituo cha Mpakani cha Namanga, Ijumaa Juni 6, alipokuwa akijaribu kuvuka kuingia Kenya.

Mwanasiasa huyo ambaye anaishi Arusha alikuwa akielekea Nairobi kwa kile alichoeleza kuwa ni uchunguzi wa kawaida wa afya yake.

Lakini kile kilichoanza kama safari ya kawaida kiligeuka haraka kuwa mzozo mkali huku maafisa wa uhamiaji huko Namanga walipomnyang'anya pasi yake ya kusafiria na kumzuia kuendelea na safari yake.

“Baada ya kuvumilia kusubiri kwa zaidi ya saa nne (4) sasa nimezuiliwa rasmi kusafiri, nimenyang’anywa hati ya kusafiria, natakiwa kurudi nyumbani Arusha,” alifunguka X.

Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini alisema ameshauriwa kuripoti Makao Makuu ya Uhamiaji Dodoma ili kupata taarifa zaidi kuhusu zuio hilo ambalo halikutarajiwa.

Katika wadhifa wake uliojaa hisia kali, Lema alisikitikia hali ya uhuru wa raia nchini Tanzania na kueleza wasiwasi wake kuhusu mustakabali wa vijana wa nchi hiyo.

"Ninatumai kwa dhati kwamba mateso haya yatakwisha hivi karibuni kwetu, na lazima tuhakikishe watoto wetu hawastahimili changamoto kama hizi maishani mwao. Hata watoto wa watesi wetu wasilazimike kuishi katika mazingira kama haya. Tutashinda," alilalamika.

Kwa nini Lema alizuiwa kusafiri kwenda Kenya

Muda mfupi baada ya taarifa ya Lema kwa umma, Idara ya Uhamiaji Tanzania ilithibitisha tukio hilo, na kukiri kuwa paspoti yake imechukuliwa na kwamba alikuwa chini ya vikwazo vya kusafiri.

Mwanasiasa wa Tanzania Azuiliwa Mpakani, Anyimwa Kiali Kuingia Kenya: "Tutashinda"
Lema alisema hati yake ya kusafiria ilichukuliwa baada ya mvutano wa saa nne katika kituo cha mpakani cha Namanga. Picha: BBC.
Chanzo: UGC

"Godbless Jonathan Lema alizuiwa kuondoka nchini na kubakizwa hati yake ya kusafiria. Sambamba na zuio hilo, Mheshimiwa Lema ameagizwa kuripoti Makao Makuu ya Uhamiaji kwa mahojiano zaidi," ilisomeka sehemu ya taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Idara hiyo, SSI Paul J. Mselle.

Idara hiyo pia ilitupilia mbali madai ya Lema kuwa viongozi wote wa CHADEMA wanakabiliwa na marufuku ya kusafiri, ikiziita taarifa hizo kuwa ni za "uongo" na kuwataka wananchi wasipotoshwe.

“Aidha, Idara ya Uhamiaji inawataka wananchi kupuuza madai ya uongo aliyoyatoa Lema kwenye mitandao ya kijamii akipendekeza kuwa zuio hili linawalenga viongozi wote wa CHADEMA,” alisema Mselle.

Tanzania ilijibu vipi lalama za makasisi

Tukio hilo linakuja huku kukiwa na uchunguzi unaoongezeka wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na jinsi unavyoshughulikia upinzani.

Jumatatu, Juni 2, mamlaka ya Tanzania ilifuta usajili wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania, linaloongozwa na Mbunge wa Kawe na Askofu Josephat Gwajima, kutokana na mahubiri yanayodaiwa kuchochea machafuko ya umma.

Msajili wa Vyama alisema kuwa meseji za Gwajima zinaweza kuibua migogoro baina ya wananchi.

Gwajima hivi majuzi alilaani kitendo cha kutekwa nyara kwa wanaharakati wakiwemo raia wa Kenya na Uganda na kuibua wasiwasi wa kutoweka kwa nguvu.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Francis Silva avatar

Francis Silva (Swahili translator) Francis M Silva ni Mkuu wa Kitengo cha Kiswahili. Ana tajriba ya miaka mingi katika taaluma ya uwanahabari hasa tafsiri, uhariri - Radio, TV na Dijitali. Yeye ni zao la Taasisi ya Mawasiliano-Umma ya Kenya (KIMC). Wasiliana naye kupitia: [email protected]

OSZAR »