Albert Ojwang’: Baba Asimulia kwa Uchungu Alivyopata Taarifa za kifo cha Mwanawe Mikononi mwa Polisi
- Meshack Ojwang Opiyo, babake marehemu mshawishi wa X, Albert Omondi Ojwang, alisimulia kwa majonzi jinsi alivyopokea taarifa za kifo cha mwanawe
- Meshack alieleza kuwa Albert alikuwa mtoto wake wa pekee, ambaye alimlea kwa taabu nyingi huku akifanya kazi kwenye machimbo ya mawe huko Pwani
- Albert alikamatwa Juni 7 na polisi waliovaa kiraia akiwa anakula chakula cha mchana nyumbani kwao Homa Bay, lakini baadaye alihamishiwa Kituo cha Central Nairobi ambako alifariki
PAY ATTENTION: Flexible Payment Plans Available! Invest in Yourself & See the Return with Our Affordable Copywriting Course!
Nairobi – Baba mwenye huzuni wa mshawishi maarufu wa X, Albert Omondi Ojwang’, amesimulia jinsi alivyopokea kwa uchungu taarifa za kusikitisha kuhusu kifo cha mwanawe.

Chanzo: Facebook
Meshack Ojwang Opiyo alisema aliambiwa moja kwa moja kuwa mwanawe alikuwa amejigonga kichwa na kufariki.
“Walisema wana habari mbaya: mwanangu alijigonga kichwa ukutani na akafariki,” alisema Meshack.
Baba huyo mwenye huzuni alielezea kwa machozi kuwa Albert alikuwa mtoto wake wa pekee. Alikumbuka mateso aliyopitia kumlea, akiwa na azma ya kumhakikishia maisha bora ya baadaye.
“Sina mwana mwingine wa kiume wala wa kike, alikuwa wa pekee. Tulihangaika sana tukiishi Pwani, nikifanya kazi kwenye machimbo kwa miaka 20 ili kuhakikisha anapata shahada,” alisema.
Kwa nini Albert Ojwang alikamatwa?
Meshack alieleza kuwa mwanawe alikamatwa na maafisa waliokuwa wamevalia kiraia siku ya Jumamosi, Juni 7, walipokuwa wakila chakula cha mchana nyumbani kwao katika eneo la Kabondo Kasipul, Kaunti ya Homa Bay.
“Mwanangu alikuwa anaangalia bustani yake ya mboga ndani ya ua wetu, nami nilikuwa nakiokota magugu kwenye shamba langu la mahindi. Baadaye alienda kufanya shughuli fulani na akarudi kwa wakati wa chakula cha mchana,” alisema Meshack.

Chanzo: Twitter
Baba huyo aliyehuzunika alieleza kuwa watu sita walifika nyumbani kwao wakiwa kwenye pikipiki tatu, hali iliyomfanya kutoka nje ili kuwakaribisha.
“Walisema wao ni maafisa wa polisi na wakasema walikuwa wanamtafuta mwanangu, ambaye kwa wakati huo alikuwa anakula chakula cha mchana akiwa nje. Walimfungia pingu papo hapo,” alieleza.
Alipouliza sababu ya kukamatwa kwa mwanawe, Meshack alisema aliambiwa kuwa Albert alikuwa amemtusi bosi wao kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).
“Nilipouliza huyo bosi ni nani, waliniambia niwafuate hadi Kituo cha Polisi cha Mawego ndipo nipate taarifa kamili. Ndugu yangu na mimi tuliwafuata na tukawakuta tayari wanaendelea kumhoji akiwa mbele ya Mkuu wa Kituo (OCS),” alisimulia.
Hata hivyo, mshawishi huyo wa mtandaoni alihamishwa baadaye hadi Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi, ambako alisajiliwa saa chache tu kabla ya kufariki katika hali ya kutatanisha.
Habari za kifo chake zilisambaa, na kuwaacha familia, marafiki na Wakenya kwa jumla wakiwa na maswali mengi kuhusu kilichompata kijana huyo akiwa mahabusu na nini hasa kilisababisha kifo chake cha ghafla.
Polisi walisema nini kuhusu kifo cha Albert?
Kwa mujibu wa ripoti ya TUKO.co.ke, Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), kupitia taarifa rasmi, ilisema kuwa Albert aliumia kichwani akiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi.
NPS ilieleza kuwa Ojwang alikimbizwa katika Hospitali ya Mbagathi ambako alitangazwa kufariki alipowasili.
Msemaji wa polisi, Muchiri Nyaga, alisema kuwa Mamlaka ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) tayari ilikuwa imeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Katika taarifa nyingine iliyotolewa Jumatatu, Juni 9, mamlaka zilifichua kuwa maafisa kadhaa wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi walikuwa wamefungiwa kazi (kuwekewa interdiction) ili kutoa nafasi kwa IPOA kufanya uchunguzi huru kuhusu tukio hilo.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke