Charles Owino Adai Mchuuzi wa Maski Aliyepigwa Risasi Aliwatukana Polisi: "Sikilizeni Kwa Makini"

Charles Owino Adai Mchuuzi wa Maski Aliyepigwa Risasi Aliwatukana Polisi: "Sikilizeni Kwa Makini"

  • Msemaji wa zamani wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Charles Owino, amezua mjadala baada ya kudai kuwa Boniface Kariuki, kijana aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi, alimtukana afisa huyo muda mfupi kabla ya tukio hilo
  • Owino alitetea huduma ya polisi na akaonya dhidi ya kuwaonyesha maafisa kama wasio na mamlaka hata katika hali za hatari
  • Kauli yake ilikuja baada ya familia ya mwathiriwa kutoa taarifa ya kusikitisha ya kitabibu huku shinikizo la umma dhidi ya polisi likiongezeka

Nairobi: Msemaji wa zamani wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Charles Owino, amedai kuwa Boniface Kariuki, kijana aliyepigwa risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi, alimtukana afisa muda mfupi kabla ya tukio hilo.

Charles Owino Adai Muuzaji wa Barakoa Aliyepigwa Risasi Aliwatukana Polisi: "Sikilizeni Kwa Makini"
Aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino alipigwa picha hapo awali (kushoto). Maafisa wa polisi waliompiga risasi Boniface Kariuki wakati wa maandamano (kulia). Picha: Muriuki Maina/Hummingbird.
Chanzo: Facebook

Kariuki alipigwa risasi kwa karibu na afisa wa polisi Klinzy Barasa alipokuwa akiuza barakoa wakati wa maandamano yaliyosababishwa na kuuawa kwa mwanablogu Albert Ojwang katika Kituci cha polisi cha Central.

Tukio hilo lilinaswa kwenye video na kusambaa kwa kasi mitandaoni, na hivyo kuchochea ghadhabu na kulaaniwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa nini polisi walimpiga risasi Boniface Kariuki?

Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV mnamo Jumatatu, Juni 30, Owino alisema:

“Ikiwa utasikiliza kwa makini video hiyo, utamsikia akimtusi afisa huyo. Ilikuwa ni mzozo mdogo tu, lakini hilo haliwezi kuwa sababu ya kupigwa risasi. Polisi wanapaswa kujizuia.”

Owino alimtetea afisa huyo, akieleza kuwa ana umri wa miaka 24 tu na ameihudumia idara ya polisi kwa chini ya miaka miwili.

Alidai kuwa Barasa alikuwa amepewa risasi za mpira—sio risasi halisi—lakini alizitumia vibaya kwa hasira za wakati huo.

Licha ya utetezi huo, Owino alikiri kwamba matukio kama hayo yanaharibu sura ya polisi na akasisitiza umuhimu wa kuwajibika.

Hata hivyo, aliendelea kuunga mkono haki ya polisi kutumia silaha katika mazingira yaliyoainishwa wazi.

“Tuna huduma moja tu ya polisi, na hatuwezi kuifanya ionekane kama adui. Ikiwa polisi atakosea, basi tuhakikishe kuwa hatua inachukuliwa dhidi yake. Lakini pia tusidanganye polisi kwamba hawawezi kutumia silaha,” alisema, akirejelea hatari wanazokumbana nazo wanapokabiliwa na umati wa watu.

“Ikiwa hatutaibua hali ya hofu, kwa mfano, pale ambapo watu 100 wanakivamia kituo cha polisi na wanajua hakuna hatua yoyote polisi watachukua, basi tunafanya nini hapa? Mtavamiwa.”

Kauli zake zimezua mjadala zaidi wakati hasira za umma zinaendelea kuongezeka kuhusu matumizi ya nguvu na polisi kupita kiasi wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

Hali ya Boniface Kariuki kwa sasa ni ipi?

Wakati uohuo, Kariuki bado yuko katika hali mahututi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Emily Wanjira, madaktari wamemtangaza kuwa amekufa ubongo, japo viungo vyake muhimu bado vinafanya kazi.

Aliongeza kuwa bili ya hospitali imepanda na kuvuka KSh milioni 3 na akaomba msaada kutoka kwa wahisani kusaidia familia kulipa gharama hizo huku wakisubiri ripoti ya mwisho kutoka kwa madaktari.

Tukio hili linaendelea kuchochea mjadala wa kitaifa kuhusu uwajibikaji wa polisi na usalama wa waandamanaji.

Charles Owino Adai Muuzaji wa Barakoa Aliyepigwa Risasi Aliwatukana Polisi: "Sikilizeni Kwa Makini"
Picha ya zamani ya Konstebo Klinzy Barasa, afisa aliyempiga risasi mchuuzi wa barakoa. Picha: Klinzy Barasa.
Chanzo: Instagram

Polisi waliompiga risasi Boniface Kariuki waondolewa kazi kwa muda

Wakati uohuo, kufuatia tukio hilo, Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS) ilithibitisha kuwa maafisa waliotajwa—Konstebo Barasa na Duncan Kiprono—waliondolewa kazi kwa muda na kwa sasa wanazuiliwa kwa sababu ya tabia yao isiyokuwa na msingi wowote.

Kesi hiyo imevutia umma kwa kiasi kikubwa, hasa kutoka kwa kizazi cha Gen Z.

Mtu mmoja muhimu katika uchunguzi huo alifichua kuwa alipokea zaidi ya jumbe na simu 1,000 kutoka kwa vijana Wakenya waliokuwa na hasira kuhusu uamuzi wake wa kuwatetea maafisa waliohusika.

Kutokana na shinikizo hilo, alijiondoa katika kesi hiyo.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »