Hisia Mseto Baada ya Moses Kuria Kuchapisha Ujumbe wa Mafumbo Kuhusu Mshindi wa Urais 2027

Hisia Mseto Baada ya Moses Kuria Kuchapisha Ujumbe wa Mafumbo Kuhusu Mshindi wa Urais 2027

  • Aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria alishiriki kile ambacho kinaweza kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2027
  • Kuria alitumia mlinganisho wa uchaguzi wa 1992 na 1997 kutabiri hatima ya Rais William Ruto katika uchaguzi ujao
  • Mipango ya Ruto kuchaguliwa tena inakabiliwa na upinzani mkali unaojumuisha aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, miongoni mwa wengine

Nairobi - Moses Kuria, mshauri mkuu wa uchumi wa Rais William Ruto, ameshiriki chapisho la kupendeza kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Hisia Mseto Baada ya Moses Kuria Kuchapisha Ujumbe wa Mafumbo Kuhusu Mshindi wa Urais 2027
Moses Kuria akizungumza katika hafla iliyopita (kushoto) na sanduku la kura za urais (kulia). Picha: Moses Kuria/IEBC.
Chanzo: Facebook

Katika chapisho la X (Twitter) Jumatatu, Mei 5, aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria alionekana kutoa dokezo la moja kwa moja kuhusu nani atakayeshinda uchaguzi wa urais wa 2027.

Nani atashinda uchaguzi wa urais wa 2027?

Katika ujumbe wake wa mafumbo, Kuria alilinganisha uchaguzi wa 2027 na chaguzi za awali za 1992 na 1997 ambazo zilishuhudia rais wa wakati huo, Daniel arap Moi, akishinda.

Kulingana na Kuria, mambo mengi hubadilika, lakini mienendo ya siasa nchini Kenya hubakia kuwa ile ile.

Aliahidi kueleza zaidi kuhusu utabiri wake katika mahojiano yajayo ya runinga, lakini Wakenya wengi waliamini alikuwa akimaanisha ushindi wa Rais Ruto.

Kuria alisema:

“Mambo yanavyozidi kubadilika, ndivyo yanavyobaki vile vile. Uchaguzi wa urais wa 2027 utakuwa na mivutano na matokeo sawa na ile ya chaguzi za 1992 na 1997. Nilikuwa katika kiini cha zote mbili, kwa hivyo najua. Nitaeleza zaidi katika mahojiano yangu ya runinga yajayo.”

Mwaka wa 1992, rais wa wakati huo Moi alishinda uchaguzi kwa kura 1,962,866.

Nani alishinda uchaguzi wa urais wa 1997?

Wagombea wakuu wa upinzani walikuwa Kenneth Matiba wa FORD-Asili (1,404,266 kura), Mwai Kibaki wa Democratic Party (1,050,617 kura), na Jaramogi Oginga Odinga wa FORD-Kenya.

Katika uchaguzi wa 1997, Moi aligombea tena kupitia chama cha KANU licha ya shinikizo kubwa la mageuzi ya uchaguzi.

Wagombea wa upinzani kama Kibaki, Raila Odinga (NDP), Michael Wamalwa (FORD-Kenya), na Charity Ngilu (SDP) waligawanyika na kukosa kuungana dhidi ya Moi, hali iliyomsaidia kushinda kwa takribani 40% ya kura.

Wakenya walivyopokea utabiri wa Moses Kuria

Hata hivyo, kauli ya Kuria ilizua mjadala mkali, huku Wakenya wengi wakikosoa na kukataa mtazamo wake.

Wengi walieleza kuwa mienendo ya kisiasa na ya wapiga kura imebadilika na kwamba upinzani unaweza kuungana ili kumshinda Ruto.

Baadhi ya maoni ya Wakenya:

CPA Peter Ndirangu:

"Lakini kuamua hata kama utashinda ugavana ni ngumu, Moses unavuka mipaka 😎"

Enock Rop:

"Acheni tu na utabiri wake. Kwa sasa, tupigie kura Prof CPA Kalunda kama mwenyekiti wa ICPAK."

Douglas Orang’i:

"Hali ya kisiasa sasa ni tofauti kabisa."

KenyaUnchained:

"1992 & 1997 zilijaa mizengwe: vurugu za kikabila, ukatili wa dola, wizi wa kura, na upinzani kugawanyika, ukamletea Moi ushindi. Kama 2027 itahisi hivyo tena, ni kwa sababu imepangwa hivyo. Wizi ule ule, matapeli wapya."

Osoro Mabuka:

"Wanasiasa wengi bado wamekwama kwa siasa za enzi za kale. Mambo yamebadilika."

@TWangatya:

"Ndio kabisa...hivi ndivyo Moi alishinda 1992 & 1997. Upinzani unakuja pamoja, unasisimka, kisha unagawanyika. Ruto anashinda. Lakini Ruto anatakiwa kuweka nguvu kwa viti vya Bunge, kwa sababu hapo atapoteza."

The Chosen African 🇰🇪🇨🇩🇭🇹:

"Ruto hawezi kushinda uchaguzi ujao, lakini tunaweza kwenda marudio ya uchaguzi."

Je, Raila Odinga atagombea urais 2027?

Wakati uohuo, katika mabadiliko ya ghafla ya kisiasa, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alidokeza uwezekano wa kutofautiana na Rais Ruto kuelekea uchaguzi wa 2027.

Hii ilifuatia kutiwa saini kwa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya ODM na chama cha UDA.

Raila, katika kauli mpya, alithibitisha kuwa chama chake kitatoa mgombea wa urais dhidi ya Ruto katika uchaguzi ujao.

Akihutubia wafuasi mjini Mombasa mnamo Jumamosi, Aprili 6, Raila alieleza wazi kuwa MoU hiyo haimaanishi ODM kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »