George Koimburi: Msimamizi wa Shamba Alikopatikana Mbunge wa Juja Afunguka, Asema Hakuwaona Watekaji
- Polisi wanadokeza kuwa madai ya kutekwa kwa Mbunge wa Juja, George Koimburi, huenda ni maigizo ya kisiasa, kwani hadi sasa hakuna ushahidi wa kuthibitisha kuwa alitekwa na maafisa wa usalama wa serikali
- Koimburi, ambaye ni Mbunge wa Juja, anaripotiwa kupatikana katika shamba la kahawa huko Kiambu baada ya siku kadhaa kupita bila kujulikana aliko
- Katika uchunguzi wao wa awali, wachunguzi wa serikali walimpata mlinzi wa shamba hilo la kahawa, ambaye alikana kushuhudia mtu yeyote akiweka mbunge huyo hapo
Polisi wanasema wanafanyia kazi kwa makini kukusanya ushahidi ili kubaini ukweli kuhusu madai ya kutekwa kwa Mbunge wa Juja, George Koimburi.

Chanzo: Facebook
Mbunge huyo anaripotiwa kupatikana bila fahamu katika shamba la kahawa lililoko Juja, siku ya Jumatatu, Mei 26.
Video ya mtaani baadaye ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonesha mbunge huyo akichukuliwa kwa gari linalodaiwa kutoka katika shamba hilo.
Alipelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Karen, ambako bado amelazwa na anapokea matibabu.
Mlinzi katika shamba la kahawa aliwaambia nini polisi?
Polisi walichukua jukumu la kuchunguza mazingira ya kutoweka kwa mbunge huyo na kurejea kwake.
Miongoni mwa watu waliowahojia ni mlinzi wa shamba hilo la kahawa linalomilikiwa na mfanyabiashara Jimmy Wanjigi.
Wachunguzi walitaka pia kulinganisha mandhari ya kahawa iliyomo kwenye video ya mtaani na ile ya shamba halisi.
Walibaini kuwa maeneo hayo hayalingani.
Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa polisi, mlinzi huyo aliwaambia kwa siri kuwa hali ilikuwa shwari katika shamba hilo na hakuonekana harakati zozote kabla au baada ya mbunge huyo kuripotiwa kupatikana.
“Tulipofika eneo la tukio lililodaiwa, maafisa wa polisi kutoka Juja walilichunguza kwa kina na kupiga picha. Baada ya kulinganisha miti ya shamba na upana wa barabara na video ya tukio, ilibainika kuwa havilingani. Wakati wa mahojiano, Moses Kariuki, ambaye ni mlinzi wa shamba la kahawa linalomilikiwa na Jimmy Wanjigi, alisema hakushuhudia tukio lolote kama hilo,” sehemu ya taarifa ya polisi ilisoma.
Ni gari gani lililotumiwa na George Koimburi?
Wakati huo huo, polisi – ambao hapo awali walikanusha kuhusika na kutoweka kwa mbunge huyo – walibaini kuwa gari lililotumika kutoka eneo alikopatikana hadi hospitali, lilikuwa ni la Koimburi mwenyewe, na kwamba mmoja wa waliomsaidia alikuwa ni dereva wake.

Chanzo: Twitter
Hata hivyo, juhudi za polisi kupata taarifa kutoka hospitali ya kwanza aliyohudumiwa Koimburi kabla ya kuhamishiwa Karen Hospital hazikufua dafu, baada ya wahudumu wa afya kukataa kutoa taarifa muhimu.
“Maafisa walielekea Hospitali ya Plainview huko Ruiru, ambako Mbunge huyo aliripotiwa kupelekwa kwa matibabu. Walithibitisha kuwa gari lililotumika, lenye nambari ya usajili KCJ 660P, lilikuwa la George Koimburi na liliendeshwa na Frida Njeri, aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika eneo la tukio lililodaiwa. Hospitali hiyo haikufichua aina ya matibabu au huduma ya kwanza iliyotolewa, jambo lililofanya iwe vigumu kubaini uzito wa majeraha aliyodaiwa kupata,” polisi walisema.
Licha ya siasa kuzingira suala hilo, polisi waliahidi kulishughulikia kitaalamu kwa nia ya kupata ukweli kamili.
Walisema pia kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na kutoweka kwa mbunge huyo atafikishwa mbele ya sheria.
“Tutaendelea kufuatilia kila dalili, kuchambua ushahidi wa kitaalamu na kuhakikisha waliohusika wanawajibika kisheria.”
Je, George Koimburi alikwepa kukamatwa?
Katika hatua nyingine, polisi walisema kuwa mbunge huyo alikuwa na taarifa kuhusu kukamatwa kwake kulikokuwa kunapangwa siku ya Ijumaa, Mei 23.
Alitakiwa kufikishwa mahakamani kwa mashitaka yanayohusiana na udanganyifu wa ardhi, kama ilivyoidhinishwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).
Kwa mujibu wa polisi, baada ya kupata habari za kukamatwa kwake, Koimburi alipanda bodaboda na kutoweka kutoka kwenye shughuli aliyokuwa anaiongoza katika eneo lake la bunge, kisha akazima simu yake.
Dereva wake alikamatwa badala yake na kupelekwa makao makuu ya DCI, ambako alitoa taarifa na kisha kuachiliwa.
Polisi walisisitiza kuwa uchunguzi wao kuhusu madai ya kutekwa kwa mbunge huyo hautahusiana moja kwa moja na mashitaka anayokabiliwa nayo.
Wandani wa Koimburi walijibu vipi taarifa ya polisi?
Baadhi ya wanasiasa kutoka upinzani walimshambulia Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, wakimtuhumu kutoa taarifa za kupotosha kuhusu kutekwa kwa Koimburi.
Waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi, alimtuhumu Kanja kwa kujaribu kufunika “utekaji wa wazi” ili kuiondolea aibu polisi.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ambaye alisema taarifa ya Kanja ilikuwa ya kusikitisha.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke