Emali:Kalonzo Abadilisha Jina la Chama kwa Heshima ya Gen Z Katika Mkutano Uliohudhuriwa na Gachagua

Emali:Kalonzo Abadilisha Jina la Chama kwa Heshima ya Gen Z Katika Mkutano Uliohudhuriwa na Gachagua

  • Kalonzo Musyoka ametangaza hadharani mchakato wa kubadilisha sura ya chama cha Wiper kwa heshima ya kizazi cha Gen Z nchini
  • Pia amewahimiza Wakenya kujipatia vitambulisho vya kitaifa kwa ajili ya usajili wa wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027
  • Kiongozi huyo wa chama ameahidi kuwa upinzani utahakikisha kwamba Rais William Ruto anahudumu kwa muhula mmoja tu

Makueni: Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amezua gumzo kwa kuzindua mabadiliko makubwa ndani ya chama chake ili kwa heshima ya vijana wa kizazi cha Gen Z nchini.

Emali:Kalonzo Abadilisha Jina la Chama kwa Heshima ya Gen Z Katika Mkutano Uliohudhuriwa na Gachagua
Kalonzo Musyoka akihutubia umma wakati wa mkutano. Picha: Kalonzo Musyoka.
Chanzo: Facebook

Tangazo kuu la Kalonzo lilitolewa wakati wa mkutano wa kisiasa uliokuwa na joto, uliohudhuriwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya Eugene Wamalwa, na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, miongoni mwa wengine.

Kwa nini Kalonzo alibadilisha jina la chama chake?

Akizungumza mjini Emali, Ijumaa, Juni 9, Kalonzo alitangaza kuwa chama chake sasa kitaitwa Wiper Patriotic Front (WPF).

Alieleza kuwa mabadiliko hayo ni heshima kwa kizazi cha Gen Z, ambacho kimeibuka kuwa nguvu kubwa nchini, hasa baada ya maandamano yao dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Kupitia kubadilisha jina la chama, Musyoka alionekana kuonyesha kujitolea kwake katika kuwawezesha vijana wa taifa.

“Wiper! Wiper! Kwa heshima ya Gen Z, sasa tunakiita chama cha WPF. Ni wangapi wanakubali jina hilo jipya? Ni wangapi wako tayari kujiunga na chama?” aliuliza Kalonzo.

Kalonzo pia aliwahimiza Wakenya kuchukua vitambulisho vyao vya kitaifa, ambavyo ni muhimu kwa ajili ya usajili wa wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Umati ulionyesha hasira zao kuhusu changamoto za kupata vitambulisho hivyo, jambo ambalo Kalonzo alisema halikubaliki:

“Wanawanyima? Tutashughulikia hilo. Tutaandika barua ya pingamizi na kuomba taarifa ya miezi 24 iliyopita kuhusu ni vijana wangapi waliopata vitambulisho.”

Aliongeza kuwa upinzani utataka maelezo ya kina ya idadi ya vijana waliopata vitambulisho, wakiwa wamegawanywa kwa jamii zao.

Kalonzo pia alisifu serikali ya Kenya Kwanza kwa kuzindua mpango wa kuhakikisha wanafunzi wa shule za sekondari wanapata vitambulisho vyao vya kitaifa:

“Natumai watafuatilia hilo. Ni muhimu kuhakikisha mwanafunzi wa Kidato cha Nne anapata kitambulisho. Hii itawawezesha kusajiliwa kama wapiga kura,” alisema.

Aidha, Kalonzo alitangaza kuwa upinzani hautavumilia wizi wa kura katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Alisisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha Rais William Ruto hatarudi madarakani, ili awe rais wa muda mmoja tu.

Je, Kalonzo alimkaribisha Gachagua nyumbani kwake kijijini?

Haya yanajiri siku chache baada ya Kalonzo kumkaribisha nyumbani kwake Tseikuru wajumbe wa upinzani wakuu, huku mazungumzo ya muungano wa uchaguzi wa mwaka 2027 yakianza kuchukua mkondo.

Emali:Kalonzo Abadilisha Jina la Chama kwa Heshima ya Gen Z Katika Mkutano Uliohudhuriwa na Gachagua
Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua nyumbani kwake Tseikuru. Picha: Kalonzo Musyoka.
Chanzo: Facebook

Miongoni mwa waliohudhuria alikuwa Gachagua, aliyewasili kwa helikopta majira ya saa tano asubuhi, akiwa ameandamana na mke wake, Mchungaji Dorcas Rigathi, pamoja na viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya.

Kabla ya kikao hicho, chama cha Wiper kilitoa taarifa kikisema kuwa mkutano huo ulikuwa na lengo la kufanya mipango ya mustakabali wa taifa.

Mkutano huo ulifanyika huku viongozi wa upinzani wakilenga kuunda muungano kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

Vichwa:
OSZAR »