Ong'ondo Were: Mahakama Yakataa Ombi la Mshukiwa wa Mauaji William Emoli Kumzika Mama Yake
- Abel Ochieng’, Edwin Odhiambo, na William Emoli Shigali wakana mashtaka ya kumuua aliyekuwa Mbunge wa Kasipul Ong’ondo Were, wakinyimwa dhamana kutokana na uzito wa kesi hiyo
- Mahakama imekataa ombi la Shigali kuhudhuria mazishi ya mama yake, Jaji Diana Kavedza akinukuu sababu za kiusalama na hatari ya mtuhumiwa kutoroka
- Upande wa mashtaka umewasilisha kesi nzito ukiwa na mashahidi 35, na kufichua kuwa washukiwa walikuwa wakwasiliana mara kwa mara na mlinzi binafsi wa Ong’ondo Were, ambaye naye anatarajiwa kufunguliwa mashtaka ya mauaji
Aliyekuwa Mbunge wa Kasipul, Ong’ondo Were, aliuawa kwa kupigwa risasi jioni ya Aprili 30, katika roundabout ya City Mortuary, Barabara ya Ngong’, na watu waliokuwa wamepanda pikipiki.

Chanzo: Facebook
Taarifa za uchunguzi zimebaini kuwa wauaji wake walikuwa wakimfuatilia kutoka Bungeni. Licha ya kuwa na walinzi, Ong’ondo alipigwa risasi mara kadhaa, risasi zikiharibu viungo muhimu ikiwemo mapafu.
Kifo chake kilishtua taifa, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa tayari ameshawahi kueleza hofu juu ya usalama wake.
Washukiwa wa mauaji ya Ong’ondo Were ni akina nani?
Baada ya kifo chake, washukiwa kadhaa walikamatwa, akiwemo mpinzani wake mkuu wa kisiasa Philip Aroko, ambaye aliachiliwa kwa dhamana kali—akiwa amepigwa marufuku kuwasiliana na familia ya marehemu, kutembelea Kaunti ya Homa Bay, na kuwasilisha taarifa polisi mara kwa mara.
Jumanne, Juni 17, 2025, washukiwa watatu wa ziada—Abel Ochieng’, Edwin Odhiambo, na William Emoli Shigali—walifikishwa mbele ya Jaji Diana Kavedza katika Mahakama Kuu ya Kibera.
Wote walikana mashtaka ya mauaji na wakanyimwa dhamana kutokana na uzito wa kosa hilo.
Jaji Kavedza alisisitiza kuwa kuwaachilia kwa sasa kunaweza kuhatarisha uadilifu wa kesi.
"Mahakama hii ina mamlaka ya kuamuru washtakiwa wasiwahi kuwasiliana wala kuingiliana na mashahidi. Endapo hilo litatokea, dhamana itabatilishwa,” alisema wakili wao, John Swaka.

Chanzo: Twitter
Sababu ya Shigali kunyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi ya mama yake
Katika ombi tofauti, Shigali aliomba apewe ruhusa ya kuhudhuria mazishi ya mama yake, lakini ombi hilo lilikataliwa.
Jaji Kavedza alisema kuruhusu hilo kunaweza kuwa mfano mbaya.
“Ombi la kuhudhuria mazishi limekataliwa kwa sababu siwezi kuhakikisha usalama wake wala kubaini iwapo yuko katika hatari ya kutoroka. Atafikaje kutoka gerezani hadi Magharibi mwa Kenya?” alihoji.
Hata hivyo, wakili Swaka alilalamikia uamuzi huo akisema, “Mazishi hayawezi kurudiwa. Kumnyima fursa ya kumuaga mama yake, ilhali hajapatikana na hatia, si haki na ni kinyume cha utu.”
Nduguye Shigali pia alionyesha masikitiko yake, akisema:
“Mama yake alifariki kwa uchungu. Lakini kwa kuwa mahakama imemzuia kuhudhuria, tunaacha yote mikononi mwa Mungu, maana Yeye peke yake ana mamlaka.”
Mwendesha mashtaka Evelyn Onunga aliitaka mahakama iendelee kuwashikilia washukiwa rumande, akitaja uzito wa tuhuma hizo.
Mashtaka yalifichua kuwa Shigali na Ochieng’ walikuwa wakiwasiliana kwa karibu na mshukiwa mwingine aliyekuwa mlinzi wa Ong’ondo Were, ambaye anatarajiwa kushtakiwa kwa mauaji katika Mahakama Kuu ya Milimani.
Kesi hiyo itatajwa tena Julai 17, 2025, kwa maelekezo zaidi. Hadi wakati huo, washukiwa wataendelea kushikiliwa.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke