Mwanamke wa Nairobi Ahuzunishwa baada ya Rafiki Kufuja Pesa Alizotuma Akiwa Kazini Lebanon

Mwanamke wa Nairobi Ahuzunishwa baada ya Rafiki Kufuja Pesa Alizotuma Akiwa Kazini Lebanon

  • Hellen Achando alitoroka nyumbani kwao kutokana na uhusiano mgumu na mamake wa kambo na akaenda kutafuta kazi kama mjakazi wa nyumbani
  • Mwanamke mmoja aitwaye Mama Docil alimchukua na kumsaidia alipobeba mimba
  • Hellen alipata kazi kama mjakazi nchini Saudi Arabia na baadaye Lebanon, ambapo alikuwa akituma pesa nyumbani mara kwa mara
  • Aliporudi nyumbani, Hellen aligundua kuwa Mama Docil alikuwa ametumia vibaya pesa zote alizokuwa ametuma kama akiba yake

Hellen Achando ameonyesha hasira na huzuni kubwa baada ya mwanamke aliyemwamini kumsaliti.

Mwanamke wa Nairobi Ahuzunishwa baada ya Rafiki Kufuja Pesa Alizotuma Akiwa Kazini Lebanon
Mwanamke wa Nairobi asema rafiki yake anayemwamini alifuja akiba yake yote. Picha: Kelvin Starbizzy.
Chanzo: Original

Alisema kuwa alilelewa na mama wa kambo ambaye hawakuwa na uhusiano mzuri. Kwa sababu hiyo, alitoroka nyumbani na akaenda kutafuta kazi kama mfanyakazi wa nyumbani huko Ruai, Nairobi.

Akiwa Ruai, alikutana na mwanamume ambaye alimpachika mimba lakini akakataa kuwajibika. Hellen alisema mwanamume huyo alimtesa, na wakati mmoja alilazimika kulala mitaani baada ya kuacha kazi na kukosa pa kwenda.

"Nilipomwambia kuwa nilikuwa mjamzito, alianza kunidharau. Nililala katika vibanda vya sokoni na vichakani mara nyingi. Ingawa wazazi wangu waliishi Nairobi, sikuweza kurudi nyumbani. Nilisaidiwa na wanawake wema waliokuwa wakinipokea kwa muda mfupi, lakini kila waliponifukuza nilirudi mitaani," alikumbuka.

Katika kipindi hicho kigumu, alikutana na mwanamke aitwaye Mama Docil ambaye alimsaidia hadi alipojifungua mtoto wake huko Zimmerman.

"Singeweza kurudi nyumbani kwa sababu mama wa kambo alinifukuza mara kadhaa nilipojaribu kurudi. Ilibidi nijikimu kivyangu," Hellen alisema.

Hellen alijaribu kazi mbalimbali nchini Kenya na hata alisafiri hadi Mombasa kufanya kazi za nyumbani, lakini mambo hayakwenda vizuri. Alirudi Nairobi na baadaye akakutana na mume wake marehemu.

"Nilikutana na mwendesha boda boda aitwaye Michael. Alinioa, na muda si mrefu nikawa mjamzito tena. Kwa bahati mbaya, alipata ajali na kufariki wakati mtoto wetu alikuwa na miezi sita pekee, na kuniacha peke yangu tena."

Mwanamke wa Nairobi Ahuzunishwa baada ya Rafiki Kufuja Pesa Alizotuma Akiwa Kazini Lebanon
Hellen Achando alirudi kutoka kazini Lebanon na kumkuta rafiki yake ametumia pesa zake zote.Picha: Kelvin Starbizzy/Hellen.
Chanzo: Original

Jinsi Hellen Alivyokwenda Saudi Arabia

Baada ya kifo cha mume wake, Hellen alikutana na rafiki aliyemtambulisha kwa mawakala wanaosaidia Wakenya kupata kazi za nyumbani nje ya nchi, hasa Saudi Arabia na Lebanon.

Alihudhuria mafunzo na hatimaye akasafiri kwenda Saudi Arabia, akimuacha mtoto wake wa kwanza kwa Mama Docil na wa pili kwa bibi ya mtoto huyo.

Alisema maisha Saudi Arabia yalikuwa mazuri, na alikuwa na mwajiri mkarimu. Hata hivyo, baadaye alianza kuugua na akaomba kurudi nyumbani.

"Nilitembelea hospitali kadhaa, lakini hali yangu haikuboreka. Nilikuwa na matatizo kwenye mguu na nilihisi kama akili yangu inazidi kudhoofika."

Subscribe to watch new videos

Baada ya kupona, Hellen aliomba kazi nyingine —safari hii nchini Lebanon—na kwa bahati nzuri aliipata haraka.

"Haikuchukua muda mrefu. Niliomba mwezi Aprili na nikasafiri Mei 2023. Nilifanya kazi kwa muda hadi niliposhindwa kuendelea."

Alieleza kuwa mazingira ya kazi Lebanon yalikuwa mabaya, waajiri wake walimnyanyasa na walikosa kumpa msaada wa kimatibabu. Aliendelea kuugua, na kila alipopelekwa hospitali, aliombwa alipe gharama, licha ya mshahara mdogo.

Wakati huu wote, Hellen alikuwa anatuma pesa kwa Mama Docil ambaye alikuwa anamlea binti yake.

"Nilimtumia takriban KSh 200,000 wakati nikiwa Lebanon. Hiyo ilikuwa akiba yangu—tofauti na pesa za matumizi ya kawaida kwa mtoto wangu."

Baada ya shambulio la mabomu Lebanon mwaka 2024, Hellen aliamua kurudi Kenya, akijilipia gharama zote za usafiri.

"Kila nilipompigia Mama Docil kumweleza jinsi maisha yalivyokuwa magumu na jinsi nilivyotamani kurudi, alinishauri nivumilie na kuendelea kufanya kazi. Sikujua alikuwa na nia fiche."

Hellen Arudi Kenya

Hellen hatimaye alirejea Kenya, lakini alipompigia Mama Docil hakupokea simu.

"Jumapili asubuhi nilienda Ruai kumtafuta. Hakuwepo. Nilikutana na binti yake wa mwisho nikamuuliza mamake yuko wapi, akaniambia alitoka kwa dharura."

Siku chache baadaye, Hellen alimkabili Mama Docil, ambaye alikiri kutumia KSh 100,000 kwa matatizo yake binafsi. Kwa hasira, Hellen alimtaka waende benki kuchukua kiasi kilichosalia.

Hata hivyo, afisa wa benki alimwambia kuwa akaunti haina hela. Kila wakati Mama Docil alipoweka pesa, alizitoa muda mfupi baadaye.

"Alichukua pesa zangu baada ya yote niliyopitia. Hilo lilikuwa jambo la kikatili. Nilikuwa sina kitu. Nilirudi kutoka Lebanon bila chochote cha kuonyesha. Niliondoka tu benki na nikamwacha hapo."

Cha kuhuzunisha zaidi, Mama Docil alimgeuza binti ya Hellen dhidi yake. Alipomjaribu kumchukua mtoto wake, msichana huyo alikataa, na Mama Docil akasisitiza hatomwachilia.

Mwanamke wa Nyahururu Alala Porini Baada ya Mamake Kumtapeli

Hapo awali, TUKO.co.ke iliripoti kuhusu mwanamke kutoka Nyahururu aliyebaki bila makazi baada ya kurejea kutoka Saudi Arabia na kukuta akiba yake yote imepotea.

Susan Wanjiru Kaigwa alisema mamake alimdanganya na kutumia KSh 500,000 alizotuma, licha ya kuwa alituma pesa za matumizi ya kila siku na karo ya mtoto wake.

Aliishia kuishi porini karibu na kaburi la babake baada ya kukosa pa kwenda.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Authors:
Shillah Mwadosho avatar

Shillah Mwadosho (Swahili editor) Shillah Mwadosho ni mwandishi wa habari wa TUKO.co.ke katika kitengo cha Kiswahili tangu 2019. Ana tajriba ya takriban miaka minne katika fani ya uandishi wa habari kwenye redio, televisheni na gazetini. Alipata ujuzi wa uanahabari katika taasisi ya Alphax mjini Eldoret. Yeye hujituliza kwa kusikiza muziki na kufurahia densi baada ya kazi. Email: [email protected]

OSZAR »