Albert Ojwang': Kituo cha Polisi cha Mawego Chachomwa Wananchi Wakiteta Dhidi ya Ukatili wa Polisi
- Umati wenye hasira ulibeba jeneza la marehemu bloga Albert Ojwang na kuzingira Kituo cha Polisi cha Mawego, ambako alifikishwa kwa mara ya kwanza kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi
- Kisha walikiteketeza kituo hicho kwa moto kabla ya kuendelea na maandamano yao katika maeneo ya karibu wakiimba kwa machungu kuhusu mauaji yake
- Picha ambazo TUKO.co.ke iliziona zilionyesha kituo cha polisi kikiwa kimechomeka kabisa huku maafisa wa polisi wakitazama kwa mbali wasijue la kufanya
Siku moja tu baada ya ibada ya wafu kufanyika kwa heshima ya marehemu mwanablogu Albert Ojwang’, wakazi wa Homa Bay walimiminika mitaani wakidai haki.

Chanzo: Twitter
Umati wenye hasira ulivamia Kituo cha Polisi cha Mawego Alhamisi, Julai 3, ambako Ojwang’ alizuiliwa kabla ya kusafirishwa hadi Kituo cha Polisi cha Central Nairobi, ambako alifariki.
Kwa hasira, walikiteketeza kituo hicho cha polisi kwa moto wakitaka haki itendeke kufuatia kifo cha bloga huyo ambaye pia alikuwa mwalimu.
Baadaye, walifanya maandamano mitaani Homa Bay wakiwa wamebeba jeneza la marehemu wakimrudisha nyumbani kwao Kasipul Kabondo.
Umati mkubwa uliowafuata waliokuwa wakibeba jeneza la Ojwang’ ulisikika ukiimba na kupiga mayowe, huenda kutokana na hasira na huzuni juu ya mazingira yaliyozingira kifo cha mwanablogu huyo.
Picha ambazo TUKO.co.ke iliziona zilionyesha kituo cha polisi kikiwa kimechomeka kabisa huku maafisa wa polisi wakitazama kwa mbali wasijue la kufanya.
Mwili wa mwanablogu huyo ulisafirishwa kwa ndege hadi Homa Bay baada ya ibada ya kumbukumbu kufanyika Nairobi. Ibada hiyo ilihudhuriwa na jamaa wa karibu na wanasiasa, wakiwemo aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi na Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya.
Wakati wa ibada ya kumbukumbu, Meshack Opiyo, baba wa Ojwang’, alitoa ujumbe mzito kwa wauaji wa mwanawe. Alinukuu hadithi ya bibilia kuhusu Kaini na Abeli, akisema kuwa damu ya mtu asiye na hatia haikomi kulilia haki.
Mazishi ya Albert Ojwang’ ni lini?
Sherehe ya mazishi ya Ojwang’ imepangwa kufanyika katika kijiji chao cha nyumbani huko Kasipul siku ya Ijumaa, Julai 4.
Kifo cha mwalimu huyo kilizua kilio kikubwa kutoka kwa umma, huku sehemu ya Wakenya wakimiminika mitaani kupinga na kudai haki. Wengine waliitaka afisa wa Naibu Mkuu wa Polisi, Eliud Lagat, ajiuzulu.
Kabla ya kukamatwa kwa Ojwang’, Lagat alikuwa amewasilisha malalamiko kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu taarifa ya kashfa iliyodaiwa kuchapishwa kwenye ukurasa wa Ojwang’ wa X (zamani Twitter).
Mkewe Albert Ojwang’ alemewa na majonzi
Tukio hili limetokea saa chache baada ya Nevnina Onyango Omondi, mjane wa Ojwang’, kutoa heshima ya mwisho kwa uchungu akimuaga mumewe.
Akionekana kulengwalengwa na machozi machoni, mjane huyo alikumbuka jinsi walivyokutana kwa mara ya kwanza na Ojwang’. Alisema walikutana kupitia rafiki wa pamoja mwaka wa 2021.
Wawili hao walibarikiwa na mtoto wa kiume ambaye sasa Nevnina amebaki kumlea peke yake. Alisema kuwa mumewe aliondoka kwa njia ya ghafla, wakati walikuwa wamepanga mambo mengi ya baadaye pamoja.
Mjane huyo aliyejaa huzuni alieleza kuwa mtoto wao mdogo hajafahamu bado kuhusu kifo cha baba yake.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke